Wema Sepetu na Mange Kimambi Wamesaidia Kukusanya Zaidi Ya Milioni 60 Kwaajili Ya Matibabu Ya Lissu
Mwanaharakati wa siasa mtandaoni Mange Kimambi na Muigizaji wa bongo movie Wema Sepetu wametajwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kama watu wanaozidi kuchangia kwenye matibabu ya mbunge wa Singida mjini Tundu Lissu.
Tundu Lissu alipigwa risasi mwezi uliopita na watu wasiojulikana akiwa mkoani Dodoma kwaajili ya kuhudhuria vikao vya bunge vilivyokuwa vinaendelea. Tangu hapo amelazwa mjini Nairobi Kenya.
Kwenye kikao alichofanya Jana na waandishi wa habari Mh. Mbowe aliwataja Mange na Wema kwa mchango wao mkubwa:
Naomba niwashukuru Watanzania wanaoishi nje ya nchi kwa michango yao ya dhati naomba nimshukuru Dada yetu Mange Kimambi anayeishi nchini Marekani kwa kuanzisha account ya ‘go fund me’ iliyowezesha kukusanya dola za kimarekani elfu ishirini na tisa na mia saba sawa na shilingi za Kitanzania milioni sitini , tunatambua mchango wa Mange na Wema Sepetu katika kuhamasisha Watanzania kuchangisha pesa hizo kupitia mitandao ya kijamii, hivyo tunapenda kuendelea kuheshimu wajibu waliochukua”.
Pia Mh. Mbowe aliwahakikishia kuwa Tundu Lissu anaendelea vizuri kwani ameshatoka ICU na sasa anakula mwenyewe bila mirija na kupumua bila oksijeni.
Mange na Wema walitumia ushawishi wao kuwaomba watu waendelee kumchangia Mh. Tundu Lissu na kwa kiasi kikubwa watu waliitikia wito na kuzidi kutoa walicho nacho.