“Nililia Machozi Ya Furaha Baada Ya Kupitia Misukosuko Mapenzini”-Mc Pilipili
Mchekeshaji maarufu Bongo Emmanuel Mathias ‘Mc Pilipili amefunguka na kuweka wazi kuwa furaha ndio iliyompelekea kuangua kilio siku chache zilizopita.
Mwanzoni mwa Wiki hii Mc Pilipili alizua gumzo baada ya kuangua kilio wakati wa kumvisha pete Mpenzi Wake Philomena Thadei huku akiwa amepiga goti.
Kwenye mahojiano aliyofanya na Gazeti la Risasi Mchanganyiko, Mc Pilipili alieleza kuwa alilia kutokana na changamoto alizokuwa amezipitia kwenye masuala ya uhusiano wa kimapenzi na msichana huyo.
Alisema hadi kufikia hatua hiyo ya kumvisha pete na binti huyo kukubali, halikuwa jambo rahisi bali alikumbana na ugumu hivyo alipoyakumbuka hayo, alijikuta machozi yakimtoka.
Nimepata misukosuko mingi sana kwenye uhusiano ndiyo maana hadi machozi yamenitoka kwa furaha kwa kuwa nimefikia hatua nzuri, natarajia kuanza vikao vya maandalizi ya harusi hivi karibuni na vitakuwa vya muda mchache kwa kuwa ninataka kufanya haraka iwezekanavyo”.
Lakini pia Mc Pilipili amesema harusi yao inategemewa kufanyika mwaka huu hapo baadaye na wanategemea kualika wageni kama 2,000.