Mwili Wa Ruge Mutahaba Kuzikwa Jumatatu Mkoani Bukoba
MWILI wa Mkurugenzi wa Vipindi Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, unatarajiwa kuwasili nchini kesho Ijumaa ukitokea nchini Afrika Kusini.
Ruge alifariki dunia Jumanne jioni akiwa huko kwenye matibabu kwa muda na kwa sasa msiba upo nyumbani kwa baba yake, Mikocheni jijini Dar.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Familia, Anick Kashasha, taratibu za kuaga mwili itakuwa ni Jumamosi.
Aliongeza kuwa Jumapili mwili huo utasafirishwa hadi Kizilu, Bukoba, kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Jumatatu.
Watu mbalimbali jana walijitokeza kutoa pole kwa familia pale Mikocheni wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi wengine wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda.
Pia wasanii wa Bongo Movie, Bongo Fleva na sanaa nyingine mbalimbali walikuwepo kutoa pole kwa wafiwa na wengine walifanya hivyo kupitia mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake Majaliwa alisema: “Historia ya Ruge kwa upande wa serikali ni kubwa, kuanzia awamu ya nne na ya tano kwa kuwatumikia kikamilifu Watanzania kwa kuwasaidia vijana wengi kielimu na msaada wake wa hali na mali.
“Ruge alikuwa balozi wa kutafsiri Philosophy ya uzalendo na fursa, vifo ni mpango wa Mungu tumuombee, salamu hizi ni kwa niaba ya serikali, kwa muda huu Rais John Magufuli anatimiza itifaki atakuja kutoa pole, tumuombee ndugu yetu.”
Naye Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba alisema kuwa:
”Uthubutu na kujituma kwa Ruge ni darasa ambalo ameliacha kwa kila mmoja aliyekuwa akimfuatilia, ubunifu na juhudi ni alama itakayodumu.”
Kala Jeremiah ambaye ni msanii wa Bongo Fleva alisema: Kuondoka kwa Ruge kutabaki kwenye kumbukumbu kutokana na namna alivyokuwa akijitoa kwa ajili ya sanaa na kuwasimamia vijana.
“Nimefanya kazi na Ruge, alikuwa mshauri mzuri mfano ni mwaka 2015 ambapo alinishauri niyatoe mashairi ya Prof. Jay kwenye Wimbo wa Nchi ya Ahadi, aliona mbele kwa kuwa Profesor alikuwa ameingia kwenye siasa ninaamini atakumbukwa daima.”
Pia Shirikisho la Soka la Tanzania kupitia kwa Rais wake, Wallace Karia, jana walionyeshwa kuguswa na msiba huo pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali. ambapo walituma salamu za rambirambi kwa wafiwa.