Mama Wema Sepetu kudaiwa kuleta masaibu mengi katika ndoa ya Msama
DAR ES SALAAM: Hatari! Mama mzazi wa muigizaji mkubwa wa filamu Tanzania, Wema Sepetu, Miriam Sepetu anadaiwa kuitikisa ndoa ya mfanyabiashara maarufu nchini, Alex Msama, Risasi Mchanganyiko limepewa mchongo mzima.
ANA KWA ANA NA CHANZO Kwa mujibu wa chanzo chetu kilicho karibu na ishu hiyo, mtikisiko huo mkubwa ulitokea ndani ya familia ya muandaaji huyo wa matamasha ya Injili baada ya mkewe kukuta ujumbe mfupi wa maneno katika simu ya mumewe, hivyo kusababisha mtafaruku.
“Sijui hasa nini kilitokea, lakini nilicho na uhakika nacho ni kuwa ndoa ya wawili hao ilikuwa katika majaribu makubwa wakati huo, maana kulionekana kuwepo kwa mawasiliano ya mara kwa mara baina ya Msama na Mama Wema, kitu ambacho mkewe alishindwa kuelewa. “Msama alijitahidi sana kupooza mambo kwa kujaribu kumuweka sawa mkewe, lakini bado ikawa ngumu hadi baadhi ya marafiki wa karibu wa pande
WAANDISHI WETU, RISASI zote mbili walipoingilia kati na kuliweka sawa jambo hilo na hivyo kupoa,” kilisema chanzo hicho. Chanzo hicho kilisema wakati mmoja katika mtafaruku huo, wanandoa hao walikuwa hawazungumzi, kitu ambacho kilitishia sana uhai wa ndoa hiyo. Baada ya kupata taarifa hizo, Risasi Mchanganyiko lilifanya juhudi kubwa za kuwatafuta wawili hao, likifika ofisini na nyumbani kwa nyakati tofauti lakini mara zote likiambulia patupu. Hata hivyo, mwishoni mwa wiki iliyopita, Msama alipatikana kupitia simu yake ya mkononi.
HUYU HAPA ALEX MSAMA
“Ni kweli, ndoa yangu ilipata mtikisiko mkubwa sana kwa sababu ya Mama Wema, mke wangu alikuta mawasiliano baina yangu na yule mama kwenye simu, akaja juu. Alikuwa akiniuliza huyu ni nani na kwa nini nawasiliana naye mara kwa mara.
“Nilikuwa nawasiliana naye mara kwa mara kwa sababu nilikuwa na biashara naye. Unajua kuna kipindi nilitaka kununua nyumba yake, nikawa wakati mwingine ninampa hela kidogokidogo, sasa katika biashara kubwa kama ile ni lazima mtakuwa mnawasiliana mara kwa mara.
“Mke wangu alipokuwa anaona meseji nyingi kutoka kwake, akawa anahisi kuna kitu, lakini nilijitahidi kumweleza kuwa ni kwa sababu ya biashara tu, hatimaye alinielewa, mambo yakaisha na sasa kila kitu kiko vizuri,” alisema Msama. Mke wa Msama ni mtangazaji wa kituo kimoja cha Redio, kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam.
VIPI KUHUSU PESA ZAKE?
Risasi Mchanganyiko lilimuuliza Msama hatima ya fedha zake za maudhiano ya nyumba ambazo hivi karibuni alilazimika kutumia Polisi ili kumkamata, baada ya kudai kuwa mama huyo alichukua fedha, lakini badala yake akamuuzia mtu mwingine.
“Hapa ni lazima niwe mkweli, siwezi kukubali huyu mama achukue tu fedha zangu kirahisi atoweke, ninasikia faili lake tayari limeshafika kwa Mwendesha Mashtaka wa serikali, ninachotaka mimi ni vyombo vya sheria kufanya kazi yake ili haki itendeke.
“Sitakubali mazungumzo, maana watu kama hawa wapo wengi sana hapa mjini, wanafanya mambo makusudi, wakitegemea huruma, siwezi kuwa na huruma na mtu ambaye anadhani udanganyifu ni jambo zuri, suala hilo ninataka limalizike mahakamani,” alisema Msama ambaye pia ni mmiliki wa Kampuni ya Habari ya Msama Media Group.
MSAKO WA MAMA WEMA
Mbio za kumsaka Mama Wema zilishika kasi na kulifikisha Risasi Mchanganyiko hadi nyumbani kwake, Sinza Mori, lakini msichana aliyefungua mlango alisema mwanamama huyo, aliyegonga vichwa vya habari wiki chache zilizopita kufuatia sakata lake na Steve Nyerere, hakuhitaji kuonana na mtu yeyote kwa wakati huo.
Kuona hivyo, waandishi wetu walimtumia ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yake ya mkononi, lakini licha ya kuonyesha kuwa ujumbe huo ulifika na kusomwa, hakurudisha majibu.
TUJIKUMBUSHE
Alex Msama na Miriam Sepetu wamejikuta wakiingia katika mtafaruku baada ya kushindwa kuelewana katika suala lao la mauziano ya nyumba ya mama huyo iliyopo Sinza Lion.
Taarifa za awali zilizoandikwa na gazeti hili, zilisema mama huyo alitaka kuiuza nyumba hiyo kwa Msama, lakini mfanyabiashara huyo alichelewesha malipo na kumfanya aiuze kwa mtu mwingine. Hadi anafikia uamuzi wa kufanya biashara na mtu mwingine, inadaiwa kuwa tayari alikuwa ameshachukua kiasi cha shilingi milioni 16 kutoka kwa Msama.
Moja kwa moja kutoka Risasi mchanganyiko