Mahakama Yaagiza Nabii Tito Apimwe Akili Upya
Mahakama ya wilaya ya Dodoma imeagiza mkazi wa mtaa wa Ng’ong’ona Manispaa ya Dodoma, Tito Machibya maarufu kama Nabii Tito kupimwa upya akili yake katika taasisi ya afya ya akili Mirembe Isanga mkoani Dodoma ili kujiridhisha kama ana ugonjwa wa akili.
Nabii Tito alijizolea umaarufu kwa mara ya kwanza kwenye mitandao ya kijamii baada ya kudai ana kanisa lake linalojulikana kama kanisa la walevi. Ambapo alifika mbali mpaka kuanza kufanya matendo machafu na wanawake mbali mbali ndipo aliposhikiliwa na jeshi la polisi mkoani Dodoma.
Hata hivyo Nabii Tito aliwekwa rumande baada ya kutaka kufanya jaribio la kujiua kwa kujikata na wembe kwenye tumbo januari 25 mwaka huu nyumbani kwake Ng’ong’ona alipokuwa anakaguliwa na polisi.
Nabii Tito alidai kuwa ana ugonjwa wa akili ndipo mahakama ilipotaka vielelezo vya daktari ili kujiridhisha kama kweli ana ugonjwa wa akili ili vitumike katika kesi yake ambapo anashtakiwa kwa kosa la kutaka kujiua au kujaribu kujiua kwa kitumia wembe.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo James Karayemaya alisema jana kuwa kutokana na mshtakiwa kuiambia mahakama kuwa ana matatizo ya akili na aliiambia mahakama kuwa alijaribu kujiua kwa sababu alisikia sauti au vitu vilivyokuwa vinamwamuru ajikate, mahakama itabidi apate uthibitisho wa vielelezo vya anachokisema hivyo mahakama imeamuru vipatikane kabla ya kesi yake haijaanza kusikilizwa. (Chanzo: Global Publishers)