Belle9 ashauri serikali baada ya kifo cha babake
Mwimbaji Belle9 alizika babake siku chache zilizopita – mzee Darmian aliaga dunia usiku wa Machi 18 baada ya kugongwa na pikipiki.
Akiongea katika kipindi cha XXL cha Clouds FM baada ya kifo cha babake, Belle alitoa ushauri kwa serikali kuhusu huduma ya PF3.
Mwimbaji huyo anasema kuwa huduma ya PF3 inachelewesha wagonjwa wengi kuikosa huduma muhimu ya kiafya inayoweza kuokoa maisha ya watu ndani ya wakati mwafaka.
Belle9 alisema haya baada ya kuenea kwa taarifa zinazodai kuwa kifo cha baba yake mzazi kilitokana na kucheleweshwa kupata huduma hospitalini.
“Mimi nadhani PF3 ingefutwa. Wangebadilisha utaratibu PF3 zitoke baada ya mtu kupata huduma ya kiafya. Kwa sababu mtu anapokuwa amepata ajali katika hali ya kawaida, anakuwa anahitaji huduma haraka, sidhani kama ni PF3 ni important sana kuliko huduma ya kiafya.
“Ijapokuwa kifo kinapotokea huwezi kukiepuka, tunaweza kutengeneza tu utaratibu ambao labda tunaweza tukapunguza vifo, hata mtu anapopata ajali, anajua anaweza akapata huduma on time,” Belle9 amekiambia Clouds FM.