Alikiba Aongelea Umuhimu Wa Kutumia Kiswahili Kwenye Nyimbo Zake Badala ya Kingereza
Mwanamuziki anayefanya vizuri kwenye Bongo fleva na kutamba na nyimbo yake ya ‘Seduce me’ Alikiba amefunguka kuwa haoni sababu ya kuacha kutumia kiswahili katika nyimbo zake inasaidia kukuza lugha yetu ya taifa na pia mashabiki ambao pia hawajui kiswahili wanaimba nyimbo zake zote.
Katika mahojiano aliyoyafanya na kituo cha televisheni East Africa Alikiba alisema haoni sababu za kutotumia Kiswahili kwani ni moja kati ya lugha kubwa sana;
“Hakuna kizuizi cha lugha kwenye muziki zamani tulikuwa tunapenda miziki ya kilingala laakini tulikuwa hatujui nini wanaimba, tulikuwa tunapenda miziki kutoka Congo lakini hatuelewi wanaimba nini bado mpaka sasa kuna watu wanapenda miziki ya kizungu lakini hawaelewi kizungu hivyo hakuna kizuizi cha lugha kwenye muziki. Kiswahili ni lugha kubwa Afrika na tunapendelea kuimba kiswahili tunakuza lugha yetu kwanza mimi najivunia kuwa mswahili nasaidia kukuza lugha yangu ya Kiswahili ifike kote inapotakiwa kufika kwasababu tayari ni lugha kubwa duniani”.
Pia Alikiba alisema haoni sababu ya kuacha kutumia Kiswahili kwa kuhofia kuwa mashabiki wake wa nchi za nje ya Afrika Mashariki hawataelewa kwani ameshafanya matamasha kwenye nchi ambazo watu hawaongei Kiswahili kabisa na bado watu wanaimba nyimbo zake pamoja na kwamba hawaelewi wanaimba nini hata kama maneno mengine wanashindwa kuyasema vizuri lakini bado wanajitahidi kuimba naye.
Kumekuwa na dhana nyingi sana ambapo wasanii wanaona bora kutumia kingereza kuimba kwenye nyimbo zao ili ziweze kusika kimataifa zaidi lakini tunasahau kuwa muziki ni sanaa ambayo inavutia kwa vitu vingi ukiachana na maneno yanayoimbwa msikilizaji anaweza kuvutiwa na biti inayotumika pia vyombo vilivyomo kwenye nyimbo na hasa sauti inayoimba kwaiyo kwa maoni yangu ni vema kuendeleza kutumia Kiswahili ili tuikuze lugha yetu ya taifa.