Mwanamke Mkenya Aganda Nyumbani Kwa Diamond Akidai Amezaa Naye
Mwanamuziki wa Bongo fleva Diamond Platnunz amerudi tena kwenye headlines baada ya mwanamke mwingine kumtuhumu kuzaa naye kisha kutekelezwa.
Mwanamke mmoja raia wa Kenya ameripotiwa kuweka kambi nje ya nyumba ya Diamond akidai kuwa hapewi pesa ya matunzo ya mtoto aliyezaa na msanii huyo. Mwanamke huyo aliyejitambulisha kama Mama Pensheni Salama anayedai kuwa raia wa Kenya aliripotiwa kukesha yeye na mtoto wake nje ya nyumba ya Diamond ikiwa ni jitihada ya kumpata msanii huyo.
Mama Pensheni alipohojiwa alieleza kuwa ni kwa muda mrefu sasa amekuwa akimtafuta Diamond bila mafanikio na amekuja Nyumbani kwake baada ya kusikia mzazi mwenza na Diamond, Zari atakuwepo nchini Tanzania hivyo ataweza kumsaidia kwani na yeye ni mwanamke kama yeye.
Walinzi wa mtaa anaoishi Diamond baada ya kumkuta Mama Pensheni amelala nje ya nyumba ya msanii huyo walimpeleka kwa mjumbe wa mtaa kwa ajili ya kumhoji. Mjumbe wa mtaa huo, Christina Chilumba alipotafutwa na kuhojiwa alikiri kuwa ana taarifa za ujio wa mwanamke huyo na kueleza kuwa mwenyekiti ndio ana taarifa zaidi kumhusu. “Ni kweli huyo mwanamke alikuja na kulala na mtoto wake pale getini kwa msanii huyo baadae alipelekwa ustawi wa jamii lakini kwa maelezo zaidi mtafuteni mwenyekiti ambaye kwa sasa yupo kikaoni yeye atawaeleza zaidi”. Aliongea Christina.
Walipomtafuta Mwenyekiti wa mtaa huo Deo akamugisha alikiri kupata taarifa za mwanamke huyo ambaye alikiri kutokea nchini Kenya na kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kumtafuta Diamond aliyedai ni baba wa mtoto wake.