Jokate Awasihi Vijana Watumie Mitandao Ya Kijamii Kutafuta Fursa
Mwanamitindo Jokate Mwegelo amewafungukia vijana wanaotumia mitandao ya kijamii kuiona Kama fursa ya kuweza kuboresha maisha yao badala ya kutumia kwa udaku tu.
Jokate aliongea hayo kwenye mahojiano aliyoyafanya na Sam Misago ambapo alitoa ushauri kwa vijana ni kwa jinsi gani wanaweza kutumia mitandao ya kijamii kuboresha maisha yao.
“Nafikiri vijana watumie zaidi mitandao ya kijamii kuweza kujielimisha kwa sababu katika ulimwengu wa sasaivi kupitia mitandao ya kijamii tumeona kuna habari nyingi ambazo zinawekwa na pia kumekuwa na fursa nyingi sana kwa vijana kwa mfano kuibuka kwa biashara kama lebo kubwa tu za nguo za nchi za nje kwasababu tu wameweza kutumia mitandao ya kijamii vizuri kwa iyo Vijana waone mitandao ya kijamii kama fursa ya biashara isiwe sehemu tu ya kupiga umbea na udaku na kutafuta umaarufu ambao hauna faida”.
Jokate aliendelea kueleza umuhimu wa mitandao ya kijamii katika biashara;
“Mitandao ya kijamii tukiitumia vizuri inaweza kutunufaisha na tukaweza kumsaidia raisi wetu kutimiza adhma yake ya kuona Tanzania inakuwa nchi ya viwanda, kwaiyo vijana tupende kujifunza kwenye hii Mitandao tuitumie tu vizuri kwa kunyanyuana zaidi ili tuzidi kuona fursa mbalimbali zilizopo kuliko kutumia kwa kupiga umbea na kufuatilia maisha ya watu binafsi”.
Jokate pia ni moja kati ya watu ambao ametumia mitandao ya kijamii vizuri kwa kufanya biashara, Jokate ambaye ni miiliki wa kampuni inayotambulika kama ‘Kidoti’ ameweza kutumia mitandao ya kijamii kuitangaza na kuikuza biashara yake.