Rockstar 4000 Wakanusha Taarifa Za Ommy Dimpoz Kuzidiwa
Uongozi wa Msanii wa Bongo fleva Omary Nyembo maarufu kama Ommy Dimpoz Rockstar 4000 umekanusha tetesi za Msanii huyo kuzidiwa.
Siku ya Jumamosi taarifa za Ommy Dimpoz kuumwa mpaka kuzidiwa ICU zilisambaa Kwenye mitandao ya kijamii na kusababisha taharuki juu ya afya ya Msanii huyo.
Kwenye mazungumzo na Mwananchi Communication Limited, siku Jumamosi Agosti 25, 2018, meneja wa msanii huyo Seven Mosha amesema hali ya msanii huyo kwa sasa inaendelea vizuri na kudai Ommy Dimpoz alifanyiwa upasuaji wa koo miezi minne iliyopita na tangu hapo hali yake imekuwa ikiendelea vizuri hadi sasa.
Juzi alikwenda hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi kwa kuwa kila baada ya miezi mitatu anatakiwa kurudi hospitali ili kuangalia maendeleo yake kama tulivyoelekezwa na madaktari.
Dimpoz ni mzima wa afya na hajalazwa, yupo nyumbani baada ya uchunguzi,” amesema na kusisitiza kuwa madaktari kutoka Hospitali ya Milpark iliyopo nchini Afrika Kusini wanamhudumia vyema”.
Baada ya taarifa za Ommy Dimpoz kusambaa siku chache zilizopita wasanii wenzake mbali mbali walijitokeza kumpa pole na kumuombea akiwemo Diamond Platnumz ambaye walikuwa hawana maelewano mazuri hapo nyuma.