Mr. Nice Achekelea Nyimbo za Wasanii Wenzake Kufungiwa
Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa Bongo fleva aliyetamba na Takeu Style miaka hiyo Mr. Nice amekuwa tofauti kidogo na watu wengine waliokasirika nyimbo 15 kufungiwa na BASATA kwani yeye amefurahia anawaunga mkono.
Wiki iliyopita nyimbo 15 za wasanii mbali mbali kama Diamond, Ney wa Mitego, Roma, na wengineo walifungiwa nyimbo zao kwa kisingizio kuwa zimekosa maadili ya Kitanzania huku Roma Mkatoliki akiambulia kufungiwa miezi Sita ya kufanya kazi.
Mr. Nice amejitokeza na kuipongeza serikali kwa hatua hiyo iliyochukua kwani amedai ni kweli nyimbo hizo hazina maadili yanayoendana na mila na desturi za Kitanzania.
Mr. Nice amefunguka hayo alipokuwa anafanya mahojiano na Planet Bongo ya East Africa redio amesema jambo hilo ni la busara kabisa kwa sababu nyimbo hizo zikiendelea kupigwa zitaharibu vijana kwa kukosa maadili:
Unajua vijana, watoto wadogo ndio wanapenda sana muziki kwa sasa, mimi kama msanii nikiimba kitu ambacho hakina maana, mantiki, adabu ni vibaya. Serikali inaona ni ajira yako lakini isifike mahali ukachafua watu wengine ni afadhali wewe samaki mmoja uliyeoza ukatupwa wengine wakaendelea kuchanua sio wote waonekane wameoza”.
Baada ya BASATA kutoa orodha hiyo ya nyimbo zilizopaswa kufungiwa na TCRA kuziweka wazi Kumekuwa na mjadala mkubwa juu ya suala hili na wasanii wengine wengi wamekemea kitendo hiki wasanii kama Fid Q, Stamina, Nikki wa pili na wengineo wengi.